SAKATA la wafanyabiashara watano waliogoma kulipa kodi ndani ya muda uliowekwa na Rais John Magufuli limechukua sura mpya baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwakabidhi kwenye vyombo vya dola kwa hatua za kisheria. Wafanyabiashara hao ni miongoni mwa 43 ambao awali walitajwa kupitisha makontena 329 bandarini bila kuyalipia kodi. Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli alitoa siku saba wajisalimishe wenyewe kulipa kodi kwa TRA bila adhabu. Akizungumza na Nipashe ofisini kwake jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo alisema kutokana na muda uliotolewa kuisha na wafanyabiashara hao kushindwa kutekeleza walichoagizwa vyombo vya dola vinaendelea kulifanyia kazi suala hilo ili hatua za kisheria zichukuliwe. Alisema wameamua kuvishirikisha vyombo vya dola kwa sababu wafanyabiashara hao wamekiuka agizo lililotolewa awali la kuwataka walipe kodi kwa hiyari yao ndani ya muda waliopewa. Alisema makampuni ya wafanyabiashara hao...