Ruka hadi kwenye maudhui makuu

CHADEMA HAIKUBALIANI NA MATOKEO YA UCHAGUZI MKUU 2015


WAKATI  Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
ikimtangaza  mshindi wa urais wa Tanzania
katika Uchaguzi Mkuu wa Jumapili iliyopita,
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kimeyakataa matokeo hayo.
Kimesema hakitakubali matokeo ya urais
yatakayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) kwa madai kuwa mchakato wa kuhesabu
kura umekiukwa na haukufuata sheria. Aidha,
chama hicho kimetaka NEC kusimamisha
kutangaza matokeo hayo kwa kuwa yako kinyume
cha utaratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana, mgombea urais wa Chadema,
Edward Lowassa alidai utangazaji wa matokeo
hayo umevurugwa na watendaji wa tume hiyo ili
kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Katika maeneo mengi ambako matokeo
yameshatangazwa mpaka sasa, kilichoripotiwa
kwa matokeo ya uchaguzi wa urais, hakifanani
wala kuendana na matakwa halisi ya wananchi.
Matokeo mengi yamesheheni udanganyifu, ulaghai
na yameandaliwa kwa lengo maalumu la kumbeba
mgombea wa CCM, John Pombe Magufuli,” alidai
Lowassa aliyepewa jukumu na umoja wa vyama
vinne vya upinzani maarufu Ukawa kuwania urais.
Alidai tangu awali uongozi wa umoja huo ulikuwa
ukitoa kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi, lakini
Tume imeendelea kutangaza matokeo hayo bila
kuchukua hatua ya kushughulikia kasoro hizo.
Alidai kuwa wanaamini wao walikuwa wana uwezo
wa kushinda kwa zaidi ya asilimia 60. “Kutokana na
makosa hayo makubwa na ya makusudi
yanayofanywa na watendaji wa NEC, mimi Edward
Ngoyai Lowassa, mgombea urais wa Jamhuri ya
Muungano na mgombea mwenza, Juma Duni Haji,
tunautangazia umma wa Watanzania na Jumuiya
ya Kimataifa, kwamba hatukubaliani na matokeo
yanayotangazwa na NEC,” alisema.
Duni ambaye kabla ya kujiunga na Chadema
alikuwa mwanachama na kiongozi wa Chama cha
Wananchi (CUF), alisema hawatakubaliana na
matokeo hayo kwa madai ya kuwa kuna kura hewa
nyingi ambazo zimeongezwa ili kuipa ushindi CCM.
Aidha, alitaka Watanzania na hasa vijana kuwa
watulivu na waendelee kuiheshimu amani iliyopo,
kwa kuwa viongozi hao bado wanajadiliana ili kujua
hatua za kuchukua.
MAHANAIMU BLOG

Maoni